Makuzi

Zitto alizaliwa tarehe 24 Septemba 1976 katika Kijiji cha Mwandiga, Wilaya ya Kigoma. Alisoma katika Shule ya Msingi Kigoma kutoka mwaka 1984 hadi mwaka 1990. Alisoma katika Shule ya Sekondari Kigoma (1991-1994) na kumalizia katika Shule ya Sekondari Kibohehe (Moshi) kati ya mwaka 1994 na 1995, akiwa amepata daraja la kwanza (Division 1:8). Alisoma katika Shule ya Juu ya Sekondari Galanos (Tanga) mwaka 1996 na kumalizia katika Shule ya Sekondari Tosamaganga (Iringa) mwaka 1998, akiwa amepata daraja la pili huku akiibuka mwanafunzi bora katika somo la uchumi katika Mkoa wa Iringa.

Zitto ana shahada ya uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliyoisomea kati ya mwaka 1999 na 2003, akiwa amepata alama 3.5 (second upper class). Zitto ana Diploma ya Juu katika Masoko ya Kimataifa kutoka Chuo cha Inwent-IHK kilichopo mjini Bonn nchini Ujerumani aliyehitimu mwaka 2004, na ana shahada ya Uzamili katika sheria na biashara kutoka Chuo cha Sheria cha Bucerius nchini Ujerumani aliyohitimu mwaka 2010.

Mwamko wa Kisiasa

Zitto alivutiwa na siasa na uongozi tangu miaka ya mwanzo tu ya ujana wake. Zitto amesoma miaka mingi zaidi kwa elimu ya sekondari na Chuo Kikuu kuliko ilivyo kawaida. Hii ni kwa sababu alipokuwa akisoma Shule ya Sekondari Kigoma alifukuzwa shule kwa kudaiwa kuwa alianzisha, kuendesha na kufanikisha mgomo yeye akiwa Kiranja Mkuu. Ndipo akalazimika kuhamia Shule ya Sekondari Kibohehe mkoani Kilimanjaro.

Aidha alipokuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Zitto alilazimika kurudia mwaka baada ya kusimamishwa masomo kutokana na kuhusishwa na mgomo wa kupinga sera ya uchangiaji wa gharama za elimu ya juu. Alikuwa ametuhumiwa kuwa alikuwa miongoni mwa viongozi waliochochea mgomo huo yeye akiwa Mwenyekiti wa wanafunzi waliokuwa wanakaa Hosteli ya Kijitonyama.

Zaidi wakati akiwa chuo kikuu cha Dar es salaam ambapo alipata malezi ya wanazuoni wa Kijamaa kama maprofesa Haroub Othman, Profesa Issa Sivji na Chachage Seithy Chachage ambao walisaidia sana makuzi yake kisiasa na kiitikadi. Alijiunga na Chadema mwaka 1992 akiwa na umri wa miaka 16 tu.

Uongozi

Kiuongozi, Zitto alikuwa Kiranja Mkuu wakati akisoma Shule ya Sekondari Kigoma na baadaye kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DARUSO) kati ya mwaka 2001 na 2003. Ndani ya CHADEMA (chama chake za zamani alichojiunga nacho 1992 mpaka mwaka 2015 alipofukuzwa), Zitto alishika nafasi kadhaa za uongozi, kwanza, alikuwa Mkurugenzi wa Mambo ya Nje mwaka 2004 na wakati huo huo akiwa pia 

Mkurugenzi wa Uchaguzi na kampeni wa chama hicho.
Zitto ameshinda Ubunge kwa mara ya kwanza akiwa na umri mdogo tu wa miaka 29 mwaka 2005 akiwawakilisha wananchi wa Jimbo la Kigoma Kaskazini kupitia chama cha Chadema. Mara baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge, Zitto alichaguliwa kuwa Katibu wa wabunge wa CHADEMA. Mwaka 2007 alichaguliwa na Baraza Kuu la CHADEMA kuwa Naibu Katibu Mkuu Bara, nafasi ambayo aliishikilia hadi mwaka 2014 baada ya kuondolewa na Kamati Kuu ya chama hicho.

Ndani ya Bunge, Zitto alipata kuwa Mwenyekiti wa iliyokuwa Kamati ya Mashirika ya Umma (POAC) na baadaye kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC). Ni katika kipindi cha uenyekiti wa Zitto, ndipo ambapo kamati hizi zilijulikana sana kwa jamii.

Kiongozi wa Chama (KC)

Zitto anaamini kikamilifu katika itikadi, falsafa na sera kama msingi wa uongozi wa kisiasa. Katika kipindi ambacho ujamaa umepoteza mashiko katika Bara la Afrika, yeye anajipambanua waziwazi kwamba ni mjamaa akiamini katika falsafa ya Unyerere.

Zitto anaamini kwamba kijiji ndiyo kitovu cha maendeleo ya Mtanzania na ni muhimu kuwekeza katika kilimo. Ndiyo mwanasiasa pekee nchini na pengine katika bara la Afrika aliyeweza kuisimamia kwa vitendo dhana ya hifadhi ya jamii kwa mwananchi wa kawaida hadi katika ngazi ya kijiji. Ni kwa sababu hii, amekuwa mwanasiasa wa kwanza barani Afrika kushinda tuzo ya hifadhi ya jamii. Zitto pia anaamini katika demokrasia rasilimali kama msingi wa kuwapa wananchi fursa ya kumiliki na kufaidika na rasilimali za taifa.

Tangu Machi 2015, Zitto ni Kiongozi wa Chama (KC) wa chama cha ACT Wazalendo, nafasi ambayo inampa jukumu la kutoa misimamo ya Kisera na Kiitikadi ya Chama cha ACT Wazalendo. Kwa sasa ni Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, na pia ni Diwani katika Halmashauri ya Kigoma Ujiji inayoongozwa na chama cha ACT Wazalendo.