Ujamaa wa Kidemokrasia
Itikadi ya ACT Wazalendo ni UJAMAA WA kiDEMOKRASIA. Kwa kuzingatia itikadi hii, Chama kinaamini katika uwepo wa demokrasia ya vyama vingi na umma kumiliki njia mkakati za uzalishaji na ambazo ni roho ya uchumi na usalama wa nchi. Aidha, tunaamini katika serikali kutoa huduma muhimu za kijamii kama vile afya na elimu kama njia ya kuleta usawa wa kibinadamu na kijamii. 

ACT Wazalendo kupitia itikadi yetu ya Ujamaa wa Kidemokrasia tuna dhamira ya kuweka mazingira ya kisera yatakayohakikisha kwamba tunapunguza pengo la kipato kati ya mtu na mtu, na kati ya jamii moja na nyingine.

.

Ngao kuu zinazoumba Itikadi ya Ujamaa wa kiDemokrasia katika mukadha wa chama chetu ni hizi zifuatazo:

Udugu ambao ni hifadhi ya jamii ya asili kwa Waafrika, tukiamini na kuhimiza katika watanzania kuishi kama ndugu na kushirikiana katika kutatua matatizo ya kijamii na kibinadamu.

Serikali kusimamia Uchumi wa nchi kwa kuwa na haki na wajibu wa kuendesha moja kwa moja sekta nyeti za kimkakati katika jamii zenye maslahi mapana ya kiusalama na kiuchumi kwa nchi bila kuathiri nafasi ya sekta binafsi kuendesha shughuli za uzalishaji mali na utoaji wa huduma.

Viongozi na watumishi wa umma wanaowajibika na wanaoenenda katika misingi ya Uadilifu na Miiko ya Viongozi. Lengo ni kuhakikisha kuwa Viongozi na watumishi wa umma wana wajibu wa kuhakikisha kwamba wanaishi na kuenenda katika misingi inayolinda heshima ya ofisi za umma na kwamba hawatumii nafasi zao kwa manufaa yao binafsi na jamaa zao.

Demokrasia ambayo ndiyo msingi wa ujenzi wa taifa huru na linaloheshimu na kuzingatia utawala wa sheria, na kichocheo cha kuibuka kwa vipaji mbalimbali miongoni mwa wananchi. Lengo likiwa ni kuhakikisha kwamba wananchi wanakuwa na fursa kikamilifu za kushiriki katika kufanya maamuzi juu ya mambo yanawagusa na kuwakabili binafsi na jamii kwa ujumla.