Uchumi Unaozalisha Ajira
Watanzania walio wengi bado wanategemea kilimo cha asili kama ajira yao. Kwa mujibu wa takwimu za Kituo cha Taifa cha Takwimu (NBS), sekta ya kilimo cha asili kinaajiri takribani robo tau (75%) ya watanzania wote. Kwa Vijijini asilimia 89 ya wananchi wanategemea kilimo wakati mijini ni asilimia 44. Kwa upande wa miji mikubwa kama vile Dar es Salaam asilimia 38 ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi wamejiajiri wenyewe au wapo katika ajira zisizohusiana na kilimo. Fursa za ajira katika mfumo rasmi bado ni finyu sana.

Tafiti zinaonyesha tatizo la ajira nchini Tanzania na nchi zingine za kiAfrika ni ukosefu wa maarifa na stadi za kazi zinazowafanya wahitimu katika ngazi mbalimbali za elimu wasiajirike. Aidha ufinyu katika sekta za uzalishaji na huduma unasababisha ufinyu wa ajira.

Ajira ni tatizo kubwa linalowakabili wananchi walio wengi nchini. Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2015, Tanzania inazalisha watu milioni 1.6 wanaohitaji ajira kila mwaka lakini ni watu elefu sabini (70,000) pekee wanaoweza kuajiriwa katika mfumo rasmi. Ili kukabiliana na ukosefu wa ajira nchini, Chama cha ACT-Wazalendo kitaendelea kupigania kuhakikisha kwamba sera mahsusi zinatungwa zitakazochochea uzalishaji viwandani na tija katika huduma za kijamii kama njia ya kupanua wigo wa ajira nchini.