[Sehemu ya Hotuba Yangu kwa Wananchi Wenzangu wa Kata ya Kagera]
Wananchi wa Kata ya Kagera, Leo pamoja na mambo mengine nitazungumza nanyi kuhusu Mradi mkubwa wa Umwagiliaji kwenye Delta ya Mto Luiche. Mradi huu upo kwenye kata yenu. Wakati wa kampeni niliwaahidi kwamba tutajitahidi kuendeleza Bonde la Mto Luiche ili kuzalisha chakula cha kutosha kwa kulisha mkoa wetu wa Kigoma, mikoa mengine nchini pamoja na nchi jirani.

Mwaka jana nilifanikiwa kupata mawasiliano kutoka Nchi ya Falme ya Kuwait kwa nchi yetu kupitia Wizara ya Mambo ya nje. Serikali ya Kuwait ilitoa dhamira yake ya kutoa fedha kuendeleza Delta ya Mto Luiche ili kuzalisha Mpunga, Mahindi na mbogamboga. Baadaye niliwasiliana na Wizara ya Kilimo na kisha Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Pia nilizungumza suala hili Bungeni mara mbili katika kuweka msisitizo wa umuhimu wa mradi huu.

Mradi huu utagharimu Fedha za kigeni USD 15 milioni sawa sawa na shilingi 31 bilioni. Fedha zote hizo Mfuko wa Wakfu wa Kuwait (Kuwait Fund) utagharamia baada ya Serikali ya Tanzania kulipia gharama za kuandaa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina (detailed design). Mwaka 2016/17 ndio nilipambana bungeni na kushirikiana na watendaji wa Kamisheni ya Umwagiliaji na Waziri wa Umwagiliaji kupata fedha hizo (za kufanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa mradi).

Bahati mbaya sana mpaka mwezi Disemba mwaka 2016, Tume ya Umwagiliaji ilikuwa imepata 13% tu ya fedha za maendeleo kutokana na Hazina kuchelewa kutuma Fedha za Maendeleo kwenye Wizara, Idara na Wakala wa Serikali. Bahati nzuri katika uchache huo wa Fedha Tume imeanza kazi ya kutimiza masharti yaliyotolewa na Serikali ya Kuwait ili kuendeleza mradi huu wa Mpunga katika Delta ya Mto Luiche. Hivyo mradi huu unaendelea na tutaupigania ukamilike.

Tutatekeleza mradi huu kwa misingi ya Ujamaa
Mradi wa Umwagiliaji wa Delta ya Mto Luiche utakuwa na ukubwa wa Hekta 2800 za Mpunga, 150 za Mahindi na 50 za mboga mboga (horticulture). Utekelezaji wa Mradi huu utafanywa kwa misingi ya itikadi na sera za kijamaa ambapo tutafanya kilimo cha Ushirika (integrated production system). 

Jumla ya familia 1400 zitagawiwa hekta 2800 za kulima mpunga ambapo kila familia itapata hekta 2 ambazo zimeshawekewa miundombinu yote muhimu ikiwemo mifereji ya maji na miundombinu ya umwagiliaji. Wakulima wataunda Ushirika na kupitia Ushirika wao watajiunga na Skimu ya Hifadhi ya Jamii ili kuweza kupata mikopo ya pembejeo, Bima ya Afya na kuweka akiba ya uzeeni.

Hakuna mwananchi aliyeko kwenye Bonde la Luiche hivi sasa ataondolewa katika utekelezaji wa mradi huu. Lengo ni kuwapa uwezo watu masikini kuondokana na umasikini wa sasa na wa baadaye kwa kupitia mfumo madhubuti wa Hifadhi ya Jamii.
Mabepari wangegawa Bonde zima kwa tajiri mmoja na kugeuza wananchi wetu vibarua wa shamba la tajiri. 

Sisi ACT Wazalendo tunawawezesha wananchi kuzalisha mali na kuendeleza maisha yao. Licha ya kutoa kipaumbele kwa wananchi wenye ardhi ndani ya Delta, mgawo wa mashamba hayo ya hekta 2 kila familia utafanywa kwa uwazi mkubwa na watu masikini watapewa kipaumbele.

Mradi wa Mpunga katika Delta ya Mto Luiche utazalisha kwa mwaka Mara 2 jumla ya tani 32,000 za mpunga kwa mwaka na hivyo kuingiza pato ghafi la takribani shilingi 16 bilioni kwa mwaka kwa wakulima kwenye ushirika wao. Huu ni wastani wa pato la shilingi 11 milioni Kwa mwaka Kwa kila familia na hivyo kuwezesha familia nyingi kuondoka kwenye umasikini na kuwa na kipato cha kati. Kupitia hifadhi ya jamii ushirika unaweza kumiliki kinu cha kukobolea mpunga na kuongeza mapato zaidi Kwa wanachama wake.

Nawataka wananchi wa Kata ya Kagera kujiandaa kuupokea mradi huu ili tuweze kujikomboa. Mradi huu utakuwa na bwawa litakalotumika kuzalisha umeme na barabara za kuelekea na kuvuka mto Luiche zitajengwa katika ujenzi wa mradi. Haya Ndio maendeleo tunayotaka Kwa wananchi wetu wa Manispaa ya Kigoma Ujiji ili tusonge mbele.

Naamini diwani wenu pia amewaeleza kuhusu utekelezaji wa mfumo wa Hifadhi ya Jamii wa Manispaa yetu ambapo tunatumia Fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo na 10% ya mapato ya manispaa Kwa Vijana na Wanawake kulipia nusu ya michango yenu kwenye Mfuko wa Hifadhi ya Jamii. Mfuko wa NSSF na Mfuko wa PSPF tayari wameanza kuandikisha vikundi vya vijana na wanawake katika Skimu yetu hii.

Wanachama watafaidika na Bima ya Afya na Mikopo nafuu kuendeleza shughuli zao za uzalishaji kupitia vikundi vyao. Nawaomba tushirikiane kujenga manispaa ambayo kila mwananchi wake ana Bima ya Afya. Inawezekana, kila mtu atimize wajibu wake.

Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Ziarani Kata ya Kagera
Manispaa ya Kigoma Ujiji 
Machi 11, 2017