Katiba
Tanzania ni zaidi ya mkusanyiko wa watu na vitu vilivyomo. Msingi wa ujenzi wa Taifa ulikuwa ni UZALENDO uliochochewa na itikadi, falsafa na imani imara. Hata hivyo, katika siku za karibuni utaifa wa Taifa la Tanzania umetikiswa. Nchi sasa imeanza kugeuka kuwa mkusanyiko tu wa watu wanaohangaika kutafuta vitu na ambao wanatumia muda mwingi kuimarisha ‘vitaifa’ vyao kupitia vyama vyao vya siasa, dini zao na hata kabila zao.

Kuna haja ya kufufua uzalendo, upendo, umoja na mshikamano wa watanzania wote bila kujali rangi, kabila, dini, jinsia na wala ufuasi wa chama cha siasa. ACT Wazalendo tunataka kufufua utaifa wa Tanzania ili kila Mtanzania aone kuwa ana wajibu wa kujenga nchi yake kwa ajili ya leo na vizazi vijavyo.
Pakua Katiba ya ACT hapa

.


Misingi ya ACT Wazalendo
ACT-Wazalendo inaongozwa na Misingi kumi ifuatayo: 

Uzalendo
Msingi wa kuanzishwa kwa Chama cha ACT-Wazalendo ni mapenzi na moyo wa dhati katika kuitumukia na kuilinda nchi yetu kwa bidii, weledi na umakini. Hivyo basi, ubora na umakini wa maamuzi yetu kama chama utapimwa kwa kuangalia ni namna gani maamuzi hayo yana faida kwa taifa letu na wananchi wake. Yaani Taifa Kwanza, leo na kesho. 

Utu
ACT Wazalendo tunaamini kwamba utu ndiyo utambulisho wa ubinadamu unaotutofautisha na viumbe vingine. Hivyo, jambo lolote tufanyalo lazima lizingatia utu na kwamba hakuna kitu chochote kinachoweza kuhalalisha kuondoa au kudhalilisha utu wa mwanadamu. Tunaunga mkono Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu na mengine yote yanayolenga kulinda utu. Aidha, tunaamini kwamba utu ndio msingi wa uhuru, haki, amani na ustawi wa jamii, na shughuli yoyote ya maendeleo ya kiuchumi, kijamii, kiutamaduni au vinginevyo lazima itangulize na kuzingatia kulinda utu na shughuli hizo hukosa uhalali pale inaposhambulia na kuvuruga utu. 

Kupinga Ubaguzi
Tunaamini kwamba kila binadamu anastahili heshima na hastahili kubaguliwa kwa sababu ya kabila, rangi, jinsi, lugha, dini, chama cha siasa, utaifa, hali ya kiuchumi, familia anayotoka, afya, ulemavu, n.k. ACT Wazalendo unaamini kwamba kila mtu anastahili kupata haki na kwamba maslahi ya makundi yote lazima yazingatiwe katika utungaji wa sera na sheria.

Usawa
Chama cha ACT-Wazalendo kimeundwa katika msingi na imani kwamba kila mtu anafurahia matunda ya bidii yake katika kazi, na kwamba bidii na umakini katika kazi ndiyo chanzo cha mafanikio kwa kila raia. Tunaamini ni jukumu na wajibu wa serikali kuhakikisha usawa katika jamii kwa kuchukua hatua stahiki za kuwainua wale ambao wapo nje ya mstari na hawafaidiki na ukuaji wa uchumi wa taifa. 

Demokrasia
Msingi mama wa demokrasia ni kuhakikisha kuwa sauti za watu zinasikika na kuzingatiwa katika mipango ya maendeleo ya nchi. Tunaamini kwamba ni wananchi pekee wenye uhalali wa kuamua nani awaongoze na aina ya viongozi wanaowataka. Kama chama, kwetu dhana ya demokrasia inakwenda zaidi ya chaguzi za mara kwa mara. Kwa ACT-Wazalendo, demokrasia ni sehemu ya mfumo wa uendeshaji wa chama ambapo kila mwanachama anayo nafasi na fursa ya kuchangia katika maamuzi ya chama na nchi, na anayo haki ya kuomba kuchaguliwa katika ngazi yoyote ya uchaguzi. 

Uhuru wa Mawazo na Matendo
Jamii yoyote ya kidemokrasia inategemea uwepo wa uhuru wa kutofautiana kimawazo na fursa ya kila mtu kutoa maoni yake bila woga. Tunaamini kwamba watu wanapaswa kuwa na uhuru wa matendo ili mradi tu matendo yao hayaingilii haki za watu wengine wala kuvunja sheria. Tunaamini kwamba ubunifu ni zao la mchango wa mawazo tofauti kutoka kwa watu tofauti. Hivyo, ACT Wazalendo tutalea na kuhamasisha utamaduni wa uhuru wa mawazo kama njia ya kuendelea kujifunza njia bora zaidi za kuboresha maisha ya watanzania.

Uadilifu
Tunaamini kwamba kura ni tendo la imani linaloonyeshwa na mwananchi kwa viongozi wanaowachagua. Uaminifu wa wananchi unapaswa kuheshimiwa kwa kuonyesha uadilifu wa hali ya juu kutoka kwa viongozi. Sisi ACT Wazalendo tutasimamia uadilifu kwa umakini mkubwa kama njia muhimu ya kujenga imani na kuwapa heshima wale wanaotuamini katika kuwatumikia. 

Uwazi
Ili wananchi waweze kuwawajibisha viongozi wao ni lazima wawe na taarifa sahihi na kwa wakati unaofaa. ACT Wazalendo tunaamini kwamba wananchi wana haki ya kupata taarifa sahihi na kwa wakati kutoka kwa viongozi wao na ofisi zote za umma kwa kuwa viongozi wanafanya kazi na kusimamia raslimali za chama na taifa kwa niaba ya wananchi.
 
Uwajibikaji
ACT Wazalendo tunaamini kwamba kila mtu anayetupigia kura ametuamini na kuweka matumaini yake kwetu kwamba tunaweza kutekeleza kile tunachosema. Tunaamini pia kwamba wanachama na viongozi wanapaswa kuwajibishwa kwa matendo na ahadi wanazozitoa kwa wananchi.

Umoja
Umoja ndiyo nyenzo muhimu ya kukabiliana na changamoto ambazo zinatukabili leo na kesho. Kama nchi ambayo imejaliwa utajiri na tofauti za kijamii mbalimbali kama vile utamaduni, kabila, dini, lugha, na siasa, tunahitaji kusimama pamoja ili kuendelea kudumisha taifa moja la Tanzania ambalo kila mmoja anafurahia kuwa sehemu yake. Aidha, kwa kuzingatia historia yetu ya kupigania umoja na maelewano katika Bara la Afrika na duniani kwa ujumla, Chama cha ACT-Wazalendo kinatambua umuhimu wa umoja na ushirikiano na majirani zetu na hivyo itashirikiana na nchi nyingine katika kusukuma mbele ajenda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya za Kikanda na Umoja wa Afrika ili kuweza kujenga nguvu za pamoja katika kujiendeleza kiuchumi, kiutamaduni na kisiasa.