Kiongozi wa Chama (KC)
Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini
Diwani wa Halmashauri ya Kigoma Ujiji

Zitto alizaliwa tarehe 24 Septemba 1976 katika Kijiji cha Mwandiga, Wilaya ya Kigoma. Zitto ana shahada ya uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ana Diploma ya Juu katika Masoko ya Kimataifa kutoka Chuo cha Inwent-IHK kilichopo mjini Bonn nchini Ujerumani, na ana shahada ya Uzamili katika sheria na biashara kutoka Chuo cha Sheria cha Bucerius nchini Ujerumani. Zitto alivutiwa na siasa na uongozi tangu miaka ya mwanzo tu ya ujana wake. Alijiunga na CHADEMA mwaka 1992 mpaka alipoondoka mwaka 2015.

Zitto ameshinda Ubunge kwa mara ya kwanza akiwa na umri mdogo tu wa miaka 29 mwaka 2005 akiwawakilisha wananchi wa Jimbo la Kigoma Kaskazini. Mara baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge, Zitto alichaguliwa kuwa Katibu wa wabunge wa CHADEMA. Mwaka 2007 alichaguliwa na Baraza Kuu la CHADEMA kuwa Naibu Katibu Mkuu Bara, nafasi ambayo aliishikilia hadi mwaka 2014 baada ya kuondolewa na Kamati Kuu ya chama hicho. Ndani ya Bunge, Zitto alipata kuwa Mwenyekiti wa iliyokuwa Kamati ya Mashirika ya Umma (POAC) na baadaye kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC). 

Zitto anaamini kikamilifu katika itikadi, falsafa na sera kama msingi wa uongozi wa kisiasa. Katika kipindi ambacho ujamaa umepoteza mashiko katika Bara la Afrika, yeye anajipambanua waziwazi kwamba ni mjamaa. Tangu Machi 2015, Zitto ni Kiongozi wa Chama (KC) wa chama cha ACT Wazalendo, nafasi ambayo inampa jukumu la kutoa misimamo ya Kisera na Kiitikadi ya Chama cha ACT Wazalendo. Kwa sasa ni Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, na pia ni Diwani katika Halmashauri ya Kigoma Ujiji inayoongozwa na chama cha ACT Wazalendo.

Wasiliana na Ofisi ya Kiongozi wa Chama ACT Wazalendo
Email: zitto@actwazalendo.or.tz
Kijitonyama, Dar es salaam