Kuasisiwa na Muundo

Chama cha Wazalendo (ACT-Wazalendo) kilianzishwa rasmi tarehe 10 Januari 2014 kwa usajili wa muda kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya siasa nchini Tanzania. Baada ya kukamilisha masharti katika kipindi cha usajili wa muda, chama kilipewa usajili wa kudumu tarehe 5 Mei 2014. Hivyo basi, kihistoria, Chama cha ACT-Wazalendo kimekuwa kikiadhimisha tarehe 5 Mei 2014 kama siku rasmi ya kuzaliwa kwake.

Kwa mujibu wa Katiba ya ACT-Wazalendo, muundo wa chama umegawanyika katika ngazi tano, ambazo ni: ACT-Tawi, ACT-Kata, ACT-Jimbo, ACT-Mkoa na ACT-Taifa. Katika ngazi kuanzia tawi hadi mkoa, viongozi wa chama ni Mwenyekiti, Katibu, na makatibu wa kamati mbalimbali. Katika ngazi ya taifa, kuna ngazi moja zaidi ambayo ni Kiongozi wa Chama (KC). Pia kuna Ngome Tatu za Chama ambazo ni ACT Ngome ya Vijana, Ngome ya Wanawake na Ngome ya Wazee.

Viongozi na Uzinduzi

Safari ya Ujenzi wa Chama cha ACT Wazalendo kinachofuata Itikadi ya Ujamaa wa Kidemokrasia iliendelea na kuchukua hatua mpya muhimu tarehe 28 Machi 2015 baada ya kufanyika Mkutano Mkuu wa kwanza ambao, pamoja na mambo mengine, ulichagua viongozi wakuu wa kitaifa, wakiwemo Kiongozi wa Chama, ndugu Kabwe Z. Ruyagwa Zitto, Mwenyekiti wa Chama Taifa, Mama Anna Elisha Mghwira, na Katibu Mkuu, ndugu Samson Maingu Mwigamba.

Pamoja na Viongozi hao, pia Mkutano Mkuu uliwachagua wajumbe wa Halmashauri Kuu pamoja na wajumbe wa Kamati Kuu. Chama cha ACT Wazalendo kilizinduliwa rasmi tarehe 29 Machi 2015 katika sherehe iliyofanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na watu 2000. 

Kushiriki Chaguzi Mbalimbali

Chama chetu kilishiriki kwa mara ya kwanza Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwezi Disemba mwaka 2014 na kupata wenyeviti na wajumbe katika ngazi za mitaa, vijiji na vitongoji. Chama kilishiriki uchaguzi mkuu wa kwanza kwa ngazi ya Urais, Ubunge na Udiwani uliofanyika Oktoba 25, 2015 ambapo Mama Anna Elisha Mghwira alisimama kama mgombea Urais huku pia tukiweza kusimamisha wagombea wa Ubunge kwa asilimia 85 ya majimbo yote nchini.

ACT ya Sasa

Katika Uchaguzi huo mkuu wa mwaka 2015 ACT Wazalendo iliweza kushinda kiti kimoja cha ubunge kwa jimbo la Kigoma Mjini, viti 42 vya udiwani katika mikoa mbalimbali nchini huku pia tukifanikiwa kushinda Halmashauri ya Kigoma – Ujiji ambayo inaongozwa na Meya kutoka chama chetu.

Kwa sasa Chama cha ACT Wazalendo kina Wanachama zaidi ya 640,000 walio katika Majimbo yote 265 ya Tanzania Bara na Zanzibar. Wanachama hao wakiwa ni Mchanganyiko wa rika, kabila, dini na matabaka mbalimbali ya Wazalendo wa Kitanzania nchini.