Azimio la Tabora
Azimio la Tabora amko rasmi la kiitikadi la Chama cha ACT-Wazalendo lilitolewa na Halmashauri Kuu ya Chama tarehe 13 Juni 2015 Mjini Tabora na kujulikana rasmi kuwa Azimio la Tabora.  Azimio hili lililenga kuhuisha Azimio la Arusha lilitolewa na Halmashauri Kuu ya Chama cha TANU Mjini Arusha tarehe 5 Februari 1967 na ambalo lilitangaza rasmi Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea nchini.
 
Umuhimu wa kuhuisha Azimio la Arusha ulitokana mambo matatu muhimu. Mosi, ni kutokana na haja ya kurejesha mambo ya msingi yaliyoasisi taifa letu, ikiwemo Umoja na Mshikamano, maadili na miiko kwa viongozi wa umma, pamoja na ari ya kujitegemea. Hii ilitokana na hali ya nchi katika siku za karibuni ambapo nyufa za ubaguzi wa kidini, kikabila, kivyama, kikanda na kimaeneo zimeanza kujitokeza na kushamiri katika Taifa letu, na hasa katika nyanja za siasa na uongozi. 

Pili, katika miaka ya hivi karibuni uongozi wa serikali na taasisi zake umetumbukia katika kashfa kubwa za ufisadi unaotishia uchumi na usalama wa nchi. Sisi katika ACT-Wazalendo tunaamini kwamba miiko ya uongozi ni moja ya njia sahihi na imara katika kudhibiti viongozi wasijitumbukize katika vitendo vya ufisadi.

Tatu, Azimio la Tabora lilitolewa kama tamko la mwelekeo wa kisera wa Chama cha ACT-Wazalendo katika kuonyesha azma yake ya kujenga uchumi shirikishi wenye kuzingatia misingi ya Ujamaa wa kidemokrasia kama ilivyoanishwa hapo juu. Ndiyo kusema, Chama cha ACT-Wazalendo kitahakikisha kwamba serikali, kwa niaba ya umma, sambamba na kuchochea fursa kwa sekta binafsi, inashiriki kikamiifu katika shughuli za kiuchumi katika sekta ambazo ni roho ya kiuchumi na kiuslama kwa nchi. Serikali haitakuwa tu mkusanya kodi bali mshiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji, sambamba na sekta binafsi.